BIASHARA United ya Mara leo inatarajiwa kushuka Uwanja wa CCM Kirumba kusaka pointi tatu mbele ya Azam FC ya Dar.
Mchezo huo awali ulipangwa kuchezwa Uwanja wa Karume ila miundombinu ya Karume haijawa rafiki.
Ikiwa inanolewa na Kocha Mkuu, Vivier Bahati imejikusanyia pointi 12 baada ya kucheza mechi 14.
Inakutana na Azam FC yenye pointi 24 ikiwa imecheza mechi 14 hivyo mechi ya leo kwa timu zote ni hesabu za kukamilisha mzunguko wa kwanza.
Ikumbukwe kwamba Bahati amewahi kuinoa Azam FC msimu huu kabla ya kuondoka pamoja na Kocha Mkuu, George Lwandamina hivyo anakutana na timu ambayo anatambua mbinu zake.
Bahati amesema kuwa wapo tayari kwa mchezo huo na kikubwa ni kuweza kupata pointi tatu muhimu.
“Tupo tayari kwa ajili ya mchezo wetu na tunatambua kwamba utakuwa na ushindani mkubwa hivyo mashabiki wawe pamoja nasi,”.
Ukuta wa Biashara United ambao umeruhusu mabao 14 upo chini ya nahodha Abdulmajid Mangalo.