KLABU ya Yanga imepunguza bei ya jezi zake ili kuwapa nafasi mashabiki wake kununua jezi za timu yao kwa bei nafuu zaidi na kuongeza hamasa zaidi.
Kauli hiyo imetolewa Februari 21, 2022 na Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara ambaye ameweka wazi kuwa malengo ya kufanya hivyo ni kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo na kuwa ni wamiliki wa jezi wa timu yao pedwa.
“Tunataka kila mechi jezi ya Yanga itawale na tumewapa heshima mashabiki wetu ili kuongeza namba ya mashabiki wanaovaa jezi uwanjani na tumetoa punguzo maalumu kwa wateja wetu wote wa jumla na rejareja.
“Tumetoa punguzo maalum la jezi kwa jumla na rejareja, rejareja sasa ni Tsh. 30,000 jumla ni Tsh. 22, 000, tunataka kuongeza hamasa kwenye viwanja vya mpira tunataka watu ‘wa-focus’ na furaha ndiyo maana tumewaletea punguzo.
“Kwa statistics (takwimu), Yanga imeuza jezi mara tano ya idadi ya jezi zilizouzwa na vilabu vyote vya ligi kuu kwa msimu huu,” amesema Manara.
Pia Omary Ally maarufu kwa jina la Marioo ameweka wazi kuwa kwa sasa yeye ni Mwananchi rasmi na amezindua wimbo rasmi wa Yanga tamu kwa kuwa Yanga ni timu kubwa na tamu.
Miongoni mwa namba ya jezi inayopendwa ni ile ya Fiston Mayele kinara wa utupiaji ndani ya Yanga akiwa ametupia mabao 6 na pasi mbili za mabao.