WATATU WA SIMBA KUACHWA

WACHEZAJI watatu tegemeo wa Simba, Chris Mugalu, Kibu Denis na Hassan Dilunga, wapo katika hatihati ya
kuongozana na msafara wa timu hiyo utakaokwenda nchini Niger.

Simba leo inatarajiwa kusafiri kuelekea Niger kuvaana na US Gendarmerie kwa ajili ya mchezo wa pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa Jumapili hii.

Katika michuano hiyo, Simba wapo Kundi D na timu za ASEC Mimosas ya Ivory Coast, RS Berkane (Morocco) na US Gendarmarie (Niger).

Taarifa zinaeleza kuwa orodha rasmi ya wachezaji watakaobaki na kusafiri na timu hiyo, itajulikana mara baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Ruvu Shooting uliochezwa Jumatano usiku na Simba iliibuka na ushindi wa mabao 7-0.

Mtoa taarifa huyo alisema hadi hivi sasa wachezaji waliondolewa katika mipango ya Kocha Mkuu, Mhispania, Pablo Franco, ni Mugalu ambaye atakuwa nje ya uwanja wiki mbili, Dilunga (nje wiki tatu) na Kibu Denis.

Aliongeza kuwa, kati ya wachezaji hao, Kibu pekee ndiye ameanza mazoezi mepesi baada ya kupona majeraha.

“Rasmi kikosi kitakachosafiri kuelekea Niger kwenda kuvaana na Gendarmarie kitajulikana mara baada ya mchezo dhidi ya Ruvu.

“Mara baada ya mchezo huo kocha ataangalia hali za wachezaji wote ili kujua kama kuna majeruhi yeyote kabla ya kutangaza watakaoondoka.

“Lakini wapo wachezaji watatu ambao wenyewe wana hatihati ya kuwepo katika msafara huo kutokana na majeraha ambao ni Kibu, Mugalu na Dilunga,” alisema mtoa taarifa huyo.

Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Hadi hivi sasa
wachezaji wenye majeraha ni Kibu, Mugalu na Dilunga.

“Majeraha hayo yamewasababishia kuukosa mchezo wa Shirikisho dhidi ya Ruvu, lakini wengine wapo vizuri akina Sakho (Pape) na Kanoute (Sadio), orodha ya wachezaji watakaosafiri kwenda Niger itajulikana hivi karibuni,” Chanzo Spoti Xtra