RAIS wa Makampuni ya GSM Group, Gharib Salim Mohammed, Jumapili aliwaalika mastaa wa Yanga nyumbani kwake Kigamboni, Dar es Salaam wakiongozwa na Fiston Mayele na Chico Ushindi kwa ajili ya kula chakula cha mchana sambamba na kufanya kikao kizito.
Yanga ambao ni mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara wakibeba ubingwa huo mara 27 ikiwa ni nyingi kuzifunika timu zote ikiwemo Simba iliyobeba mara 22, msimu huu inaongoza msimamo wa ligi kwa kukusanya pointi 36 ikicheza mechi 14.
Licha ya kuwa kileleni kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Simba yenye 31, lakini Yanga imekuwa na presha kubwa ya kuzidiwa ujanja na wapinzani wao hao na kuukosa ubingwa.
Mmoja wa mabosi wa Yanga, amesema kuwa, Gharib aliwaalika nyumbani kwake mara baada ya kumaliza program ya mazoezi ya asubuhi.
Bosi huyo alisema kuwa, wakiwa huko, walifanya kikao kilichoandaliwa maalum kwa ajili ya kuwaongezea hamasa mastaa hao ili wafanye vema katika michezo ya ligi pamoja na Kombe la Shirikisho la Azam Sports.
Aliongeza kuwa, kikao hicho pia kiliwahusisha viongozi wa Benchi la Ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu Mtunisia, Nasreddine Nabi na baadhi ya viongozi wa Kamati ya Utendaji wa Yanga.
“Kikao kilikuwa na malengo mazuri ya kuijenga timu na zaidi kuwaongezea hamasa na morali wachezaji ili wapambane katika michezo ijayo.
“Gharib alipata nafasi ya kuzungumza na mchezaji mmoja mmoja hapo nyumbani kwake baada ya kikao cha pamoja ambapo kuna maagizo maalum wachezaji wamepewa.
“Hii siyo mara ya kwanza kwake kufanya kikao na wachezaji chenye lengo la kuwaongezea morali na kufahamu majukumu yao ya uwanjani ili wafanikishe malengo ya kuchukua ubingwa,” alisema bosi huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alizungumzia hilo kwa kusema: “Mara kwa mara uongozi tumekuwa tukifanya vikao na wachezaji, kikubwa ni kuwakumbusha majukumu yao ya uwanjani, kama unavyofahamu malengo yetu msimu huu ni kuchukua ubingwa katika michuano tunayoshiriki.”