>

MO AWAWEKEA SIMBA MIL 200 WAIFUNGE ASEC

 

KATIKA kuhakikisha wanapata ushindi wa kwanza nyumbani dhidi ya Asec Mimosas ya nchini Ivory Coast katika mchezo wa kwanza wa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Rais wa Heshima wa Simba, bilionea Mohamed Dewji ‘Mo’, ameahidi kuwapa bonasi nzuri inayofikia Sh 200Mil kama wakifanikiwa kuwafunga wapinzani wao hao.


Timu hizo zinatarajiwa
kuvaana Jumapili hii saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.


Simba ambao ni wenyeji
katika mchezo huo, watawakosa wachezaji wake muhimu wenye majeraha Chris Mugalu, Kibu Denis na Clatous Chama ambaye kanuni zinambana kucheza michuano hii kutokana na
kucheza mechi za michuano
ya Caf akiwa na RS Berkane ya Morocco.


Bosi huyo juzi alivamia
kambi ya timu hiyo iliyopo Bunju, nje kidogo ya Dar es Salaam, saa chache kabla ya
kuelekea mazoezini kwa ajili
ya kuzungumza na wachezaji hao.


Mara baada ya kuvamia
kambini hapo alifanya kikao na wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wakiwemo
Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya timu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’,


Mtendaji Mkuu, Barbara
Gonzalez na mjumbe wa bodi, Mramu Ng’ambi. Chanzo chetu kimetudokeza kuwa katika kikao hicho, Mo alitoa ahadi hiyo ya bonasi kama wakifanikiwa kupata ushindi wa nyumbani dhidi ya Asec.

“Morali ya wachezaji itaongezeka katika kuelekea mchezo wetu dhidi ya Asec ni baada ya maneno mazuri
waliyoambiwa wachezaji
wetu na Mo ambaye ni mwekezaji wetu.


“Wachezaji wote
walihimizwa kupambana katika mchezo huu ili kuhakikisha tunafuzu katika
hatua hii na kufuzu kufika
nusu fainali, wachezaji chini ya nahodha Bocco (John) walitoa ahadi nzito kwa Mo
na kuahidi kupambana kupata
ushindi.


“Ahadi hiyo ya Mo
imeongeza morali kwa kila mchezaji aliyepo kambini,” kilisema chanzo hicho.

MO AFUNGA KUELEKEA MCHEZO HUO
“Mimi nimetoka mbali na
hii Simba, nashangaa hao watu wanaosema kuwa mimi nimeondoka Simba, nilianza
kuipenda timu hii tangu
nikiwa mdogo.


“Nimewekeza pesa nyingi
ndani ya Simba nilianza kwa kuweka Sh 25Bil lakini kabla nilikuwa nilishatumia
20Bil kabla ya kuongezea Sh
20Bil, hivyo hadi hivi sasa nimefikisha 85Bil ambazo nimetumia katika kipindi
changu nikiwa na timu.

“Lipo wazi kuiendesha klabu kubwa kama ya Simba ni hasara, lakini naendelea kutoa pesa zangu kwa ajili
ya Simba, hivyo mimi nipo
Simba.


“Tuliteleza kidogo katika
msimu huu na kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia huku Shirikisho,
malengo yetu ni kufika mbali
zaidi ya hapa tulipofikia.

“Tunafahamu tuna majukumu mengi, ikiwemo ligi lakini ninaamini tutapambana, ni lazima  tujipange kwani haya
mashindano ni magumu na
siriazi.

 

“Bado tunaendelea kupambana na bajeti yetu ya Simba ili timu iweze kujiendesha yenyewe na kwa miaka minne niliyokuwa kiongozi ndani ya Simba ambayo hivi sasa sina mamlaka nayo sana baada ya kujiondoa katika nafasi ya mwenyekiti wa wakurugenzi, lakini bado nipo ndani ya timu kwa ajili ya kuwasaidia, hivyo niwaambie kuwa nitaendelea kuisadia timu yangu ya Simba.


“Lengo ni kuweka bajeti
kubwa ndani ya timu hiyo ili tuweze kupambana na baadhi ya klabu kubwa katika
Ukanda wa Afrika kama vile
Al Ahly.


“Wengi wanasema
mafanikio ya Simba ni Mo lakini mimi naamini mafanikio ya Simba ni mashabiki. Wajitokeze kwa
wingi Jumapili. Kiingilio
cha chini ni Sh 5,000 lakini natangaza kushusha hadi Sh 3,000,” alisema Mo.