BODI YA LIGI KUU BARA YAFUNGUKIA HATMA YA GSM

MWENYEKITI wa Bodi ya Ligi Kuu Bara, Steven Mnguto, ameibuka na kusema licha ya wadhamini wenza Kampuni ya GSM kutangaza kujiondoa katika udhamini lakini hakuna klabu yoyote iliyolipwa.


Kauli hiyo
imekuja ikiwa ni siku moja tangu GSM watangaze kujiondoa kudhamini klabu za ligi ambazo awali waliingia mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 2.1Bil.


Akizungumza
na Championi Jumatano, Mnguto alisema kuwa, hilo suala wamepanga kulizungumza hivi karibuni
mara baada ya Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) watakapokutana.


Mnguto alisema kuwa,
wanasubiria wanasheria wao walipitie suala hilo na mwisho wa siku watalitolea ufafanuzi
kwa undani.


“Kiukweli tangu tuliposaini
mkataba na GSM nikiri klabu hazijapata chochote. Klabu zimeitangaza GSM kwa muda wa miezi mitatu sasa, kwa hiyo tunasubiri wanasheria walipitie suala hilo tujue tunafanyaje.

 

“Hata suala la zile nembo kwenye mabega sijui kama zinaweza kutolewa haraka lakini hata hilo litafanyiwa
kazi kisheria,” alisema
Mnguto.

 

Naye Mkurugenzi wa Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura, akizungumzia hilo alisema: “Sisi
baada ya kupata
barua kutoka GSM, suala la mkataba ni Bodi ya Ligi na ni vema akatafutwa Mnguto lakini
kwa upande wa
sisi TFF hatuwezi kuzungumzia kila jambo.


“Tayari tumetoa tamko letu
jana (juzi) kuhusiana na hilo baada ya kupata barua GSM.” Juzi TFF ilitoa taarifa
kuwa, Februari 7, mwaka huu
walipokea barua ya kuvunja mkataba wa udhamini mwenza wa Ligi Kuu Bara
ya NBC kutoka Kampuni ya
GSM, hivyo Shirikisho hilo linafanyia kazi barua hiyo na litatoa taarifa kwa wadau.