>

MO APIGA HESABU ZA UBINGWA KIMATAIFA SIMBA

MWEKEZAJI katika Klabu ya Simba, Mohammed Dewji, ‘Mo’ amesema kilicho mpeleka kambini leo ni mapenzi yake kwa Simba na amekutana na viongozi wachezaji kwa ajili ya kuwapa hamasa kuelekea mchezo dhidi ya ASEC ya Ivory Coast.

Mo ameweka wazi kuwa malengo makubwa kwa Simba ni kuweza kuona inafanya vizuri kitaifa na kimataifa kwa kubeba makombe makubwa ili kuongeza heshima.

Mo Dewji amesema wakati huu wapo katika Kombe la Shirikisho Afrika lazima wajipange kwa sababu ni mashindano ya kweli ila bado wanakazi ngumu kwenye ligi na lazima kuwa na malengo makubwa.

“Ukweli kwanza kuwekeza ndani ya Simba ni hasara bado tunapambana sana kuifikisha Simba katika bajeti kubwa ya kujiendesha yenyewe, katika miaka minne nilikuwa kiongozi ila sasa hivi sina mamlaka yoyote.

“Nipo pamoja sana na Mwenyekiti, Salim Abdalla ‘Try Again’, Bodi ya Wakurugenzi pamoja na mashabiki kuendelea kuisaidia timu ili kuwa na bajeti kubwa kushindana na klabu kama Al Ahly.

“Unajua Simba ni klabu kubwa Afrika na tunatakiwa kuwa na muendelezo wa kucheza robo, nusu fainali mara kwa mara ya mashindano ya kimataifa lakini la pili Super Cup sina taarifa nalo ila viongozi wakubwa wa Simba walienda Misri katika mkutano na bado hawajanipa feedback yoyote.

“Naamini kwamba mafanikio ya Simba ni mashabiki na wiki hii tuna mechi ngumu na wakijitokeza watu 3,5000, Mungu atujalie hizo pointi tatu tutapata na nitakuwepo uwanjani, kwani bila ya mashabiki hakuna Simba wala Mo Dewji.

“Kitu ambacho tunataka awamu hii ni kuvuka katika hatua ya robo fainali na kuweka historia kwani wachezaji nao wataingia kwenye historia ya Tanzania na ya Simba kitu ambacho tunataka tusonge mbele zaidi kwani ipo siku nao watasema wameitumikia Simba tushinde ubingwa wa Afrika na kombe la Shirikisho Afrika,” amesema Mo Dewji.