SHABAN Kazumba, Kocha Msaidizi wa Tanzania Prisons, amesema kuwa bao la penalti ambayo walipata Simba ni halali kwa kuwa ilitolewa na mwamuzi kutokana na makosa ambayo walifanya.
Bao hilo lilifungwa na Meddie Kagere na lilionekana kuwa na utata kutokana na wachezaji wa Prisons kumfuata mwamuzi kulalamika juu ya penalti hiyo.
Kazumba aliliambia Championi Jumamosi kuwa:-“Simba wamepata penalti, kwangu penati ni sehemu ya makosa siwezi kusema kwamba tumefungwa kwa bao la penalti hapana siwezi kusema kwamba namlaumu mwamuzi.
“Kwangu naona liko sahihi lakini kidogo naona ilikuwa ni kwa wepesi kwetu,lakini tumefungwa tunakubali matokeo tumepoteza pointi tatu na timu yangu ilicheza mpira ule unaopendwa na Kocha Mkuu Patrick Odhiambo ambaye anapenda kuona timu inacheza mpira mzuri.
“Tulikosa nafasi tatu za kufunga mbele ya Simba na tulikuwa tunajua kwamba tunacheza na mabingwa, Simba alistahili na mchezo wa mpira ni mgumu sana,” alisema Kazumba.
Prisons ipo nafasi ya 16 ikiwa na pointi 11 huku Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 28 kibindoni zote zimecheza mechi 14.
Ilikuwa ni Februari 3 ambapo Simba iliweza kusepa na pointi tatu Uwanja wa Mkapa na viungo wa Simba ambao walianza kwenye mchezo huo ilikuwa ni pamoja Rally Bwalya huku pembeni alikuwa ni kijana Israel Mwenda aliyekuwa akipambana katika kutimiza majukumu yake.