UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa malengo yao makubwa msimu huu ni kuhakikisha wanashinda michezo mingi kadiri inavyowezekana ili kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo na kukata tiketi ya kucheza mashindano ya kimataifa msimu ujao.
Azam ambayo ipo chini ya kocha Abdi Hamid Moallin, ipo nafasi ya tatu na pointi zake ni 24 kibindoni.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’ amesema “Tunajua wazi kuwa ligi ya msimu huu ni ngumu na kama klabu kila mtu anajua ni namna gani tulipitia kipindi kigumu mwanzoni mwa msimu huu, lakini kwa sasa tumerekebisha sehemu kubwa ya mapungufu tuliyokuwa nayo.
“Malengo yetu makubwa ni kuhakikisha tunashinda michezo yetu ijayo kadiri itakavyowezekana ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushiriki mashindano ya Afrika msimu ujao,”.
Vinara wa ligi ni Yanga wakiwa na pointi 36 kibindoni huku wanafuatiwa na Simba wenye pointi 28 wakiwa nafasi ya pili.