CHICO WA YANGA APEWA KAZI HII KIKOSINI

PAMOJA na mashabiki wa Yanga kuendelea kuwa na shauku ya kutaka kumuona winga wao mpya raia wa DR Congo, Chico Ushindi akifanya mambo yale aliyokuwa akiyaonesha enzi hizo akiwa na TP Mazembe, unaambiwa kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi, kumbe anamuandaa kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.


Winga huyo amejiunga 
na Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15, mwaka huu akitokea TP Mazembe.

Chanzo chetu kutoka katika kambi ya Yanga iliyopo Avic Town, Kigamboni, Dar, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, malengo ya Nabi ni kumtumia zaidi Chiko katika mzunguko wa pili wa ligi, hivyo kwa sasa anajitahidi kuhakikisha anampa nafasi ya kuzoea mazingira ili aje kuongeza nguvu katika mbio za kuwania ubingwa.

“Ukiambiwa usajili wa kocha wetu Nabi siyo wa kukurupuka basi huna haja ya kubishana na hilo, kwani hadi sasa anadhihirisha kwa Chico Ushindi ambaye amemsajili hivi karibuni kutoka TP Mazembe, kwani amesema hana haraka ya kumpa presha badala yake ataendelea kumuingiza katika mfumo wake taratibu mpaka pale atakapozoea.


“Malengo yake siyo 
kumuona Ushindi akicheza tu, ila anahitaji kumpa muda mzuri wa kurejea katika ubora wake kwani alikotoka alikuwa hapati nafasi mara kwa mara, hivyo anamuandaa kwa ajili ya mzunguko ujao ambapo wachezaji wengi huwa wanakumbwa na majeraha,” kilisema chanzo hicho.


Hivi karibuni, Nabi 
alimzungumzia kiungo huyo akisema: “Ninaamini uwezo wa Ushindi uwanjani, hivyo hilo sina hofu nalo kabisa, usajili wake mimi ndiyo nilioupendekeza, ni suala la muda tu kuonesha ubora wake.”


Yanga imebakiwa 
na mechi mbili kukamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara ambapo inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 35.