PANCHA YAKWAMISHA MIPANGO YA KMC KUTUSUA KIMATAIFA

HITIMANA Thiery, Kocha Mkuu wa KMC ameweka wazi kuwa miongoni mwa sababu ambazo zimewafanya washindwe kusonga mbele katika hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Shirikisho ni pamoja na tatizo la pancha ambalo liliwakuta wakiwa njiani.

Kutolewa kwa timu hiyo katika hatua hiyo kumeyeyusha ndoto ya timu hiyo kuweza kuipeperusha Tanzania kimataifa kwa sababu bingwa wa Kombe la Shirikisho hupata nafasi kuiwakilisha Tanzania kimataifa.

KMC ilifungashiwa virago kwenye hatua ya 32 bora na Ruvu Shooting kwa kupata penalti 5-6 walifunga Ruvu Shooting baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Azam Complex kusoma KMC 1-1 Ruvu Shooting.

Thiery amesema kuwa mpango mkubwa ulikuwa ni kupata matokeo chanya kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.

“Ninaweza kuzungumza msafara tulifanya ulikuwa mrefu tulitoka kama saa sita kasoro hivi tukapata pancha njiani tukakaa na kutafuta gari jingine na kufika saa tisa  hivi tukiwa tumechelewa na tulifika na kuingia kuanza mazoezi moja kwa moja hivyo ilifanya wachezaji kuwa wamechoka.

“Kipindi cha kwanza tulikuwa na kipindi cha kucheza na tulipata bao lakini kipindi cha pili tulishindwa kucheza vizuri wakaweza kusawazisha. Kwa upande wa penalti hakuna mwenyewe hizo hazina fundi lakini kilichotokea ni kwamba tumetolewa,” amesema Thiery.

Kwa KMC ni Idd Kipagwile alitupia bao dakika ya 24 na lile la kuweka usawa kwa Ruvu Shooting ilikuwa ni kupitia kwa Abrahman Mussa kwa pigo huru dakika ya 61 lililomshinda Tanzania One, Juma Kaseja.