MOHAMED Makaka kipa namba moja wa Ruvu Shooting anaingia kwenye orodha ya makipa wa kazi chafu kutokana na uwezo wake wa kuokoa mashuti yasiweze kuingia kwenye lango lake.
Mastaa wa Simba wakiongozwa na Meddie Kagere bado watakuwa wanajua balaa la mikono yake licha ya Simba kushinda kwa mabao 3-1 bado Makaka alikuwa mhimihili kwa timu yake kwa kuweza kuzuia michomo 7 iliyokuwa inakwenda langoni mwake.
Imekuwa ni kawaida ya Makaka kutimiza wajibu wake kwani hakuweza kufanya maajabu Novemba 19 pekee mbele ya Simba hata walipokutana na Yanga alifanya maajabu ilikuwa Novemba 2,2021, Uwanja wa Mkapa aliweza kuokoa michomo 7 ya Fiston Mayele pekee.
Pia rekodi nyingine ya Makaka kwenye mechi za vigogo hawa wawili aliweza kuokota mabao nyavuni mara sita na kila mechi ilikuwa inapatikana penalti ambapo mbele ya Yanga alifungwa na Djuma Shaban na mbele ya Simba aliokoa penalti iliyopigwa na Erasto Nyoni.
Alipata tabu Uwanja wa Mabatini mbele ya Kagera Sugar ambapo alifungwa bonge moja ya bao lililompa maumivu wakati akiwa kwenye harakati za kuokoa mchomo huo mkali uliopigwa nje ya 18.
Ruvu Shooting ikiwa imecheza mechi saba amecheza mechi zote akiwa na clean sheet,(cheza bila kufungwa) mbili.