KOCHA MPYA SIMBA AANZA KAZI RASMI LEO

LEO Novemba 16, Kocha Mpya wa Viungo wa Klabu ya Simba, Don Daniel De Castro ameanza kazi ya kuwanoa wachezaji wa timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Pablo Franco.

Kocha huyo wa viungo amechukua mikoba ya Adel Zraine raia wa Tunisia ambaye alisitishiwa mkataba wake Desemba 26.

Jana, Novemba 15 alitambulishwa rasmi kwa mashabiki na kukaribishwa kwenye familia ya Simba ambao ni mabingwa watetezi.

Kwenye mazoezi ya leo yaliyofanyika Uwanja wa Boko Veteran, kocha huyo alikuwa akishirikiana na makocha wote wa Simba wakiongozwa na Pablo kuwapa maelekezo wachezaji wa timu hiyo.

Wengine ni makocha wasaidizi, Seleman Matola na Hitimana Thiery waliokuwa na kazi ya kuwapa malekezo vijana hao wa Msimbazi walio nafasi ya pili na pointi 11 baada ya kucheza mechi tano.

Kwa sasa timu hiyo inajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Pablo anatarajiwa kuwa na kbarua cha kwanza Novemba 19 Mwanza kusaka pointi tatu mbele ya Ruvu Shooting.