MILTON Nienov, raia wa Brazil aliyekuwa kocha wa makipa ndani ya Klabu ya Simba amebainisha kuwa alikuwa amesaini dili jipya la kuendelea kuitumikia timu hiyo mpaka 2024 ila haikuwa hivyo baada ya mabosi wa timu hiyo kuamua kuvunja mkataba wake.
Nienov alikuwa akimnoa kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula, Beno Kakolanya, Jeremia Kisubi na Ally Salim hivyo amefungashiwa virago vyake akiwa hajakamilisha hata mwaka mmoja baada ya kusaini dili jipya.
Ni Oktoba 26 rasmi ilitangazwa kwamba hatakuwa sehemu ya kikosi hicho ambacho kwa sasa kipo chimbo kumsaka mbadala wake ambaye atakuwa na kazi ya kuwanoa makipa hao wa Simba.
Kocha huyo amesema:”Mwezi Agosti nilisaini mkataba mpya kwa ajili ya kuendelea kuitumikia Simba na mkataba wangu ulikuwa unakwenda mpaka mwaka 2024 hivyo unaweza kuona namna gani nimeweza kuutumia mkataba wangu kwa muda.
“Hivyo unaweza kuona kwamba nimetumia miezi mitatu pekee katika mkataba wangu mpya, kuondoka kwetu kumetushangaza na nimepokea ujumbe mwingi kutoka kwa mashabiki wa Simba ambao wanaonekana hawaelewi kilichotokea,”.
Chanzo:Spoti Xtra