Ally Kamwe Asema Yanga Imejiandaa: “Kesho Tunakwenda Kutafuta Heshima Yetu”

Msemaji wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe, amesema kuwa licha ya baadhi ya watu ndani ya makundi ya wapenzi wa soka kuitazama Yanga kama timu dhaifu katika mchezo wao ujao dhidi ya AS FAR Rabat, kikosi cha Yanga kimejipanga kikamilifu kwenda kuonesha ubora wao na kutafuta heshima uwanjani.

Akizungumza leo kuelekea mchezo huo muhimu unaotarajiwa kuchezwa kesho, Kamwe amesema timu hiyo imekuwa ikitazamwa kwa dharau na baadhi ya wachambuzi, jambo alilosema halina mashiko kutokana na maandalizi waliyofanya.

“Kwenye kundi letu watu wanaiona Yanga kama vile saidia fundi, lakini wachezaji wataenda kutuheshimisha,” alisema Kamwe akijibu mitazamo ya wanaodai kuwa Yanga ndiyo timu iliyo chini kwenye ubora ndani ya kundi hilo.

Kamwe amesisitiza kuwa maandalizi ya timu yako katika hatua ya mwisho na kila mchezaji yuko tayari kupambana kuhakikisha wanapata matokeo chanya dhidi ya mabingwa wa Morocco, AS FAR.

Aidha aliongeza kuwa dhamira ya Yanga ni kufanya vizuri si tu kwa ajili ya mashabiki wao, bali pia kwa heshima ya timu na bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Mchezo huo dhidi ya AS FAR Rabat unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa, huku Yanga ikilenga kupata pointi muhimu ili kuongeza nafasi ya kusonga mbele katika hatua za michuano hiyo.