JKT Queens wawakilishi wa Tanzania katika anga la kimataifa kwa timu ya Wanawake Septemba 14 2025 itakuwa kibaruani kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali.
Ni JKT Queens vs Kenya Police Bullets mchezo huo unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Kasarani, ikiwa ni hatua ya nusu fainali.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa JKT Tanzania, Masau Bwire ameweka wazi kuwa nusu fainali hiyo itatanguliwa na nusu fainali ya kwanza kati ya Rayon Sports Women ya Rwanda dhidi ya Kampala Queens ya Uganda.
Ameongeza kuwa tayari kikosi cha JKT Queens asubuhi kimefanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo ambapo mazoezi wamefanyika katika Uwanja wa Don Bosco, Caren, Nairobi.
Kuhusu hali za wachezaji amebainisha kwamba wote ni wazima, hakuna majeruhi na wote wana morari ya kutosha kwa ajili ya mchezo huo.
Kwa upande wa wachezaji wenye mabao mengi ni Jamila Rajabu anaongoza kwa idadi kubwa ya magoli, amefunga magoli manne, akiwa mchezaji pekee aliyefunga magoli matatu katika mchezo mmoja.
Masau amewaomba Watanzania kuendendelea kuwaombea ili wafuzu mchezo wa kesho wa nusu fainali, ili wafike fainali na hatimaye kuwa mabingwa wa mashindano hayo.
Haya ni Mashindano ya CAF, ligi ya mabingwa Wanawake, ukanda wa CECAFA, 2025, yanayoshirikisha timu tisa kutoka katika mataifa mbalimbali, yanaendelea Nairobi, nchini Kenya ikiwa ni hatua ya makundi.
Timu tisa zinashiriki mashindano hayo ni pamoja na bingwa mtetezi CBE (Ethiopia), Kenya Police Bullets (Kenya), Kampala Queens (Uganda) na YEI Joint Star (Sudan Kusini).
Nyingine ni JKU Princess (Zanzibar), Denden WFC (Eritrea), Top Girls Alliance (Burundi), Rayon Sports Women (Rwanda) na mabingwa wa mashindano hayo mwaka 2023, JKT Queens (Tanzania).
Timu hizo zimegawanywa katika makundi matatu, A, B na C, kila kundi likiwa na timu tatu.
Kundi A, lina timu za Kenya Police Bullets, Kampala Queens na Denden WFC, kundi B, linaundwa na timu za CBE, Top Girls Alliance na Rayon Sports Women, wakati kundi C linajumuisha timu za JKU, YEI Joint Star na JKT Queens.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, katika hatua ya nusu fainali, mshindi wa kundi A atacheza na mshindi wa kundi C na mshindi wa kundi B atakutana na timu itakayopata matokeo mazuri (best losser).
Imeandikwa na Masau Bwire, Ofisa Habari JKT Tanzania.