Mwanza, Julai 28, 2025 – Klabu ya Pamba Jiji FC imetangaza kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba na kocha wao mkuu Fred Felix Minziro, baada ya pande zote mbili kuridhiana kuhitimisha ushirikiano wao.
Taarifa rasmi ya klabu imethibitisha kuwa hatua hiyo imefikiwa kwa mazungumzo ya amani, bila mvutano wowote, na kwamba uongozi unatoa shukrani kwa Kocha Minziro kwa mchango wake katika maendeleo ya timu hiyo katika kipindi alichokinoa kikosi hicho.
Fred Minziro, ambaye pia ni mmoja wa makocha wenye uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania, amekuwa na klabu hiyo katika kipindi cha mabadiliko na kujenga kikosi chenye ushindani katika ligi za ndani.
Katika taarifa hiyo, klabu ya Pamba Jiji imeeleza kuwa tayari imeanza mchakato wa kumtafuta kocha mpya ambaye atakiongoza kikosi hicho kuelekea msimu ujao wa mashindano, huku ikilenga kuimarisha kikosi na kuongeza ushindani katika ligi.
Mashabiki wa Pamba Jiji sasa wanatazama kwa hamu kuona ni nani atakayekabidhiwa jukumu la kuiongoza timu hiyo, huku matarajio yakiwa juu kwa msimu wa 2025/2026.