Dar es Salaam, Julai 28, 2025 – Klabu ya Yanga SC imetangaza rasmi kumsainisha kiungo mshambuliaji wake, Maxi Mpira Nzengeli, nyongeza ya mkataba mpya wa miaka miwili, hatua itakayomuweka klabuni hadi mwaka 2027.
Maxi Nzengeli, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ameonyesha kiwango bora tangu ajiunge na Yanga mwaka 2023 akitokea klabu ya Union Maniema. Katika kipindi cha misimu miwili aliyokaa Jangwani, Nzengeli amekuwa mchezaji tegemeo katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, akichangia mabao na pasi muhimu za mabao kwenye michuano ya ndani na kimataifa.
Uongozi wa Yanga umethibitisha kuwa mkataba huo mpya ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha kikosi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya CAF Champions League, ambako klabu hiyo inaweka malengo ya kufika hatua za juu zaidi.
Kwa sasa, Maxi anatarajiwa kujiunga na kikosi kilicho kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2025/2026, huku mashabiki wa Yanga wakifurahia uamuzi wa klabu kumbakiza moja ya wachezaji wao walioweka alama ndani ya timu.