MAN UNITED YAMNYAKUA MBEUMO KUTOKA BRENTFORD KWA DAU LA REKODI

Manchester United imefikia makubaliano na Brentford kumsajili winga wa kimataifa wa Cameroon, Bryan Mbeumo, kwa dau la pauni milioni 65, linaloweza kupanda hadi pauni milioni 70 kutokana na nyongeza ya pauni milioni 5.

Mbeumo, mwenye umri wa miaka 25, anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kabla ya kujiunga rasmi na kikosi cha kocha Ruben Amorim, ambacho kinapangwa kuelekea Marekani Jumanne ijayo kwa ziara ya maandalizi ya msimu mpya.

Huu utakuwa usajili wa tatu wa United katika dirisha hili la majira ya joto, baada ya kuwasili kwa mshambuliaji Matheus Cunha na beki wa kushoto Diego Leon.

United ilianza kwa kuwasilisha ofa ya pauni milioni 55 mapema mwezi Juni, ambayo ilikataliwa. Ofa ya pili ya pauni milioni 62.5 pia haikukubaliwa, lakini Brentford hatimaye wamekubali dau la sasa, likiwa ni la juu zaidi kuwahi kulipwa kwa mchezaji wao tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo.

Mbeumo alijiunga na Brentford mwaka 2019 akitokea Troyes ya Ufaransa, na amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu waliowasaidia The Bees kudumu katika Ligi Kuu ya England. Uhamisho huu unamfanya kuwa mchezaji aliyeuzwa kwa gharama kubwa zaidi katika historia ya Brentford.