DIOGO JOTA AFARIKI DUNIA KATIKA AJALI MBAYA HISPANIA

Mchezaji wa kimataifa wa Ureno, Diogo Jota, aliyekuwa na umri wa miaka 28, amefariki dunia mapema leo asubuhi, Julai 3, 2025, katika ajali mbaya ya gari iliyotokea kwenye mkoa wa Zamora, nchini Hispania.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya Hispania na Uingereza, ajali hiyo imetokea katika eneo la Palacios de Sanabria na Cernadilla, ambako gari alilokuwa akisafiria lilitoka barabarani na kushika moto. Katika ajali hiyo pia, ndugu yake mdogo, André Silva, ameripotiwa kupoteza maisha.

Jota, ambaye alikuwa akiichezea klabu ya Liverpool FC, alikuwa ameoa hivi karibuni mnamo Juni 22, 2025, na ameacha mjane pamoja na watoto wake watatu. Kifo chake kimesibitishwa rasmi na mamlaka za Hispania na Ureno, na tayari wimbi la huzuni na mshtuko limesambaa duniani kote, hasa kwenye jamii ya soka.

Wachezaji wakubwa, vilabu vya soka, mashabiki na viongozi wa serikali mbalimbali wametoa rambirambi zao kwa familia ya Jota, mke wake, watoto, na taifa la Ureno.

Diogo Jota atakumbukwa kama mshambuliaji mahiri, mwenye nidhamu, upendo wa familia na mapenzi ya dhati kwa mchezo wa soka. Alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Liverpool na timu ya taifa ya Ureno, akitoa mchango mkubwa katika mafanikio ya vilabu na nchi yake.