Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma, amepongeza uongozi wa Rais mstaafu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodgar Tenga, akisema kuwa ametoa mchango mkubwa katika kuendeleza michezo nchini na kwamba ni kiongozi wa kuigwa.
Akizungumza wakati wa mjadala wa bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Musukuma amewataka viongozi waliopo madarakani kujifunza kutoka kwa Tenga jinsi ya kuongoza michezo kwa weledi na uzalendo.
Aidha, Musukuma amehoji kuhusu kutokuwepo kwa mrejesho wa kikao kilichofanyika kati ya Waziri wa Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), wakiongozwa na Rais Wallace Karia, pamoja na Bodi ya Ligi. Kikao hicho kilifanyika kufuatia kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi, Yanga dhidi ya Simba, iliyokuwa ichezwe tarehe 8 Machi 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.