Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amefariki dunia leo Jumatatu akiwa na umri wa miaka 88, hatua inayofunga ukurasa wa uongozi wake uliojaa changamoto, migawanyiko na juhudi za kulifanyia mabadiliko Kanisa hilo la miaka 2,000. Vatican imethibitisha taarifa hizo kupitia video iliyosambazwa kwa vyombo vya habari.
“Ndugu wapendwa, kwa huzuni kuu nawasilisha taarifa ya kifo cha Baba Mtakatifu Francis. Saa 1:35 asubuhi leo, Askofu wa Roma, Francis, amerejea nyumbani kwa Baba,” amesema Kardinali Kevin Farrell kupitia televisheni ya Vatican.
Papa Francis, ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio, alikuwa papa wa kwanza kutoka Amerika Kusini. Alichaguliwa rasmi mnamo Machi 13, 2013, katika hatua iliyowashangaza wengi waliomwona kama mtu wa nje katika duru za Vatican, kutokana na mtazamo wake wa kuwa karibu na maskini na kuishi maisha ya unyenyekevu.
Tofauti na waliomtangulia, Papa Francis hakuwahi kuhamia katika jumba la kifahari la upapa (Apostolic Palace), akisema kuwa maisha ya kijumuiya yalikuwa muhimu kwa afya yake ya kisaikolojia.
Katika kipindi chake, alikumbana na changamoto nzito ikiwa ni pamoja na kashfa ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto ndani ya Kanisa na migawanyiko katika uongozi wa Vatican. Aliteuliwa na Baraza la Makardinali kwa dhamira ya kurekebisha hali hiyo.
Hata hivyo, alikabiliwa pia na upinzani mkali kutoka kwa wahafidhina waliomshutumu kwa kuvuruga mila na utaratibu wa muda mrefu wa Kanisa hilo. Wakati huo huo, baadhi ya watu wa mrengo wa mbele walihisi kuwa hakufanya juhudi za kutosha kulifanyia mabadiliko Kanisa hilo.
Licha ya hayo, Papa Francis alijijengea heshima na umaarufu mkubwa kimataifa kwa ujumbe wake wa amani, mshikamano wa kidini, na kutetea wanyonge – hususan wakimbizi, wahamiaji na jamii zilizotengwa.
Kufikia Februari 2025, Papa Francis alikuwa amewateua karibu asilimia 80 ya makardinali wenye haki ya kupiga kura kumchagua Papa ajaye – hali inayoweka uwezekano wa mrithi wake kuendeleza mwelekeo wa sera zake za mageuzi.