BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeazimia mambo manne kuhusu Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwamo kuhakikisha ukarabati wake unakamilika ifikapo Aprili, 2025.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko ameyasema hayo leo bungeni alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo.
Sekiboko amesema serikali iandae mkakati wa kuanzisha chombo maalum cha usimamizi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa na viwanja vingine vinavyojengwa na Serikali ili kuhakikisha vinatunzwa na kuwa katika ubora wa kimataifa.
“Serikali iweke utaratibu wa sehemu ya makusanyo ya uwanja kubaki kwa matumizi ya uwanja huo ili kurahisisha matengenezo ya dharura yanapojitokeza na iandae mkakati wa kuboresha viwanja vingine vya michezo ili kupunguza mzigo wa matumizi makubwa kwa Uwanja huo,”—amesema.
Awali bi Sekiboko alisema uwanja wa Benjamin Mkapa ni moja ya miundombinu muhimu ya michezo nchini inayotumiwa kwa matukio ya kitaifa na kimataifa, lakini unakabiliwa na changamoto za matengenezo na usimamizi endelevu.