JONATHAN IKANGALOMBO KUWAKOSA KEN GOLD KESHO

Kuelekea mchezo wa Ligi Kuu bara kati ya wenyeji Yanga Sc dhidi ya Ken Gold Fc utakaopigwa kesho Februari 05, 2025 katika dimba la KMC Complex, kocha wa Yanga, Sead Ramovic amesema winga Mkongomani, Jonathan Ikangalombo Kapela aliyesajiliwa dirisha dogo kwa sasa hawezi kutumika kwa sababu hana utimamu mzuri wa mwili.

“Jonathan ni mchezaji mzuri sana, jambo la kwanza tunalopaswa kufanya, bila shaka, ni kumfikisha kwenye kiwango cha utimamu wa mwili tunachotaka. Kwa sababu si tu kuhusu utimamu wa mwili, bali pia kuhakikisha kwamba hapati majeraha”

“Ikiwa hana utimamu wa kutosha na anahitaji kukimbia kwa kasi kwenye mechi, kuna uwezekano mkubwa wa kuumia, na hilo ndilo tunalotaka kuepuka. Lakini bila shaka yeye ni mchezaji mzuri na katika siku zijazo atatusaidia sana” — amesema kocha huyo raia wa Ujerumani.