Miquissone Arudi Kwa Kishindo, Aipa Ud Songo Taji Baada Ya Miaka Mitatu

Winga wa zamani wa Simba SC na Al Ahly ya Misri, Luis Miquissone, ameandika ukurasa mwingine muhimu katika safari yake ya soka baada ya kufunga hat-trick na kuiongoza União Desportiva do Songo (UD Songo) kutwaa taji la Ligi Kuu ya Msumbiji (Moçambola 2025).

Katika mchezo huo uliochezwa dhidi ya GDR Textáfrica do Chimoio, UD Songo iliibuka na ushindi mkubwa wa mabao 5-1, ushindi uliowafanya watangaze ubingwa rasmi wa msimu huu.

Miquissone alifunga mabao yake dakika ya 8, 12 na 38, akionesha kiwango cha juu kilichowafanya mashabiki wa UD Songo kuendelea kumuenzi kama mmoja wa wachezaji muhimu katika historia ya klabu hiyo. Hat-trick hiyo ilimaliza kabisa matumaini ya wapinzani na kuwahakikishia mabingwa hao pointi muhimu walizohitaji.

Ushindi huo umeifanya UD Songo kutimiza pointi 59 katika michezo 22, ikiwa na pengo la pointi 19 mbele ya Black Bulls wanaoshika nafasi ya pili, japokuwa wana michezo miwili mkononi — tofauti ambayo haiwezi kufungwa.

Baada ya kumaliza kazi klabuni, Miquissone sasa anaelekea kwenye majukumu ya kimataifa, ambapo anatarajiwa kukiongoza kikosi cha Msumbiji katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika nchini Morocco.

Ushindi huu unarejesha heshima ya UD Songo katika soka la Msumbiji na pia unaonesha upekee wa ubora wa Miquissone ambaye anaendelea kung’ara ndani na nje ya mipaka.