
JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema linachunguza tukio la ajali ya gari kumgonga mwendesha pikipiki na kusababisha kifo, tukio lililotokea Novemba 14, 2025 usiku huko eneo la Kipera kata ya Mkundi Manispaa ya Morogoro.
Taarifa ya leo Novemba 16, 2025 iliyotolewa na Kamanda wa Poliai Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama imeeleza kuwa gari namba 04 JU 0157 mali ya TFS Morogoro lililokuwa likiendeshwa na Nicholaus Simba (38) dereva na mkazi wa Morogoro liliigonga pikipiki yenye namba za usajili MC 139 DDB aina Haojue ikiendeshwa na Edmund Edward Temba (39) mkulima na mkazi wa Tubuyu9Tubuyu9 na kusababisha kifo chake papo hapo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni uzembe wa dereva wa gari kushindwa kuchukua tahadhari kiasi cha kusababisha kumgonga mwendesha pikipiki na kusababisha kifo chake kabla ya dereva huyo wa gari kutoroka kusikojulikana.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema linaendelea na uchunguzi zaidi ili kumkamata mtuhumiwa huku likiendelea kuwaelekeza madereva kuchukua tahadhari zote na kuzingatia sheria ya usalama barabarani ili kukoa na kulinda maisha ya watumiaji wote wa barabara.
