Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtaka Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kutumia nafasi aliyopewa kuwatumikia Watanzania wote bila upendeleo wa aina yoyote.
Akizungumza leo Novemba 14, 2025 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kumuapisha Dkt. Mwigulu, Rais Samia alisema nafasi hiyo ni ya kitaifa na siyo ya marafiki, ndugu au jamaa.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akiapa Kiapo cha Maadili kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 14 Novemba, 2025.
“Mzigo huu si mdogo kwa umri wako, mzigo huu ni mkubwa. Kwa umri wako vishawishi ni vingi vya marafiki, ndugu na jamaa. Nafasi yako ile haina ndugu, haina rafiki, haina jamaa; ni nafasi ya kulitumikia taifa hili,” alisema Rais Samia.
Aidha, alimtaka Waziri Mkuu mpya kuhakikisha anaweka mbele maslahi ya wananchi na kusimamia kwa uadilifu majukumu yote aliyokabidhiwa.