Yanga Yaonywa na Bodi ya Ligi Kwa Kuvunja Ratiba ya Mchezo

Klabu ya Young Africans imepewa Onyo Kali kwa kosa la kushindwa kufuata ratiba ya matukio ya mchezo (match countdown) kuelekea mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar Fc uliomalizika kwa Yanga Sc kuibuka na ushindi wa 2-0 kwenye uwanja wa KMC Complex Oktoba 28, 2025, hatua ambayo ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Taarifa ya Novemba 11, 2025 iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu imeeleza kuwa Young Africans walishindwa kuwasilisha leseni za wachezaji wao kwa wakati jambo lililochelewesha zoezi la ukaguzi, ambapo ililazimika lifanyike saa 9:44 alasiri badala ya saa 8:50 mchana kama ratiba ilivyoainisha.