KUELEKEA kwenye mchezo wa marudiano CAF Champions League, Oktoba 25 2025 uongozi wa Yanga SC umeweka wazi kuwa mechi hiyo itakuwa mikononi mwa mashabiki baada ya kuomba wapewe hilo jukumu.
Hiyo imetokana na mashabiki wengi kufunga safari kuelekea nchini Malawi kuishangilia timu hiyo Oktoba 18, 2025 kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Bingu matokeo yaliposoma Silver Strikers 1-0 Yanga SC.
Yanga SC inahitaji ushindi wa angalau goli 2-0 katika mchezo wa Oktoba 25,2025, Uwanja wa Mkapa huku mashabiki wakiombwa kuwa wastaarabu na wasifanye vurugu yoyote ile wala kuwasha moto wakiwa uwanjani.
Ali Kamwe Ofisa Habari wa Yanga SC amesema kuwa wanachama wa Yanga SC waliomba mechi ya Jumamosi kusiwe na viingilio jambo ambalo limefanyiwa kazi na uongozi kwa umakini mkubwa na kuamua iwe hivyo.
“Tumepokea maoni mengi kutoka kwa Wanachama wetu wakiuomba uongozi wa Yanga kuwa mechi ya jumamosi usiwe na viingilio, tuwaachie wao mchezo huu na tuwape nafasi ya wao kuisapoti timu yetu na kuivusha kwenda hatua ya makundi.
“Tayari uongozi wetu umekutana na kujadili maoni haya ya wanachama na kimsingi wamelipokea, wamekubaliana na kulipitisha ombi hili la Wanachama wetu. Hivyo ombi limekubaliwa na mashabiki wawe makini kwenye mchezo wetu wasilete vurugu.