Yanga SC vs Wiliete SC Septemba 27 2025 Uwanja wa Mkapa

ALI Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga SC amesema kuelekea mchezo wa kimataifa dhidi ya Wiliete leo Uwanja wa Mkapa kauli mbiu ni Mfumo Umekubali.

Yanga SC Septemba 27 2025 ina kazi ya kusaka ushindi kwenye mchezo wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni mchezo wa marudio.

Ipo wazi kwamba katika mchezo wa kwanza ugenini nchini Angola Yanga SC ilipata ushindi wa mabao 3-0 hivyo ina kazi ya kulinda ushindi huo kusonga mbele hatua inayofuata katika anga la kimataifa.

Kamwe ameweka wazi kuwa wanatambua ushindani uliopo na namna wapinzani wao walivyo imara, wataingia kwa tahadhari kupata matokeo mazuri.

“Tumekuja na kauli mbiu ya Mfumo Umekubali ikiwa ni maalum kwa ajili ya mchezo dhidi ya Wiliete tu. Tuna jambo la tofauti mtaliona mkija uwanja wa Mkapa. Kuna moto mkali sana utawashwa.

“Tunaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kwa kuwa hata upande wa viingilio tumeona namna itakavyokuwa rafiki. Kumbukwa kwamba mashabiki wetu wana nidhamu kubwa kweli.

“Uongozi wetu umeweka kiingilio rafiki sana eneo la mzunguko kuwa ni Tsh 3000 tu, na hii ni kuhakikisha tunakuja kwa wingi tuweze kuishangilia timu yetu. Tiketi kwenye majukwaa mengine ni VIP C 10,000, VIP B 20,000 na VIP A ni 30,000.”