Simba SC vs Gaborone United kupigwa Uwanja wa Mkapa Septemba 28

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba SC kesho wanakibarua cha kusaka ushindi kwenye mchezo wa hatua ya awali ambao utakuwa wa marudio dhidi ya Gaborone United ya Botswana.

Katika mchezo wa kwanza ugenini Simba SC ilipata ushindi wa bao 1-0 mfungaji akiwa ni Ellie Mpanzu kwa pasi ya Shomari Kapombe. Septemba 28 2025 mchezo wa marudio unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa bila ya uwepo wa mashabiki.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC amesema kuwa wanatambua umuhimu wa mchezo huo licha ya kutokuwepo na mashabiki wachezaji watapambana kutafuta matokeo.

“Tunafahamu ya kwamba tuna mechi ya Ligi ya Mabingwa siku ya Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa kuanzia saa 10 jioni na tayari wageni wetu Gaborone United wamewasili. Mambo yote yamekwenda vizuri.

“Mchezo wetu wa Jumapili utachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Niger na sasa wapo njiani. Kikosi kiliingia kambini  baada ya mchezo dhidi ya Fountain Gate walirudi kambini na wapo timamu, hakuna mtu yeyote ambaye alipata majeraha. Watakaokosa mchezo ni Mohammed Bajaber na Abdulrazak Hamza.

“Nipo hapa kuwathibitishia kwamba mechi yetu ya Jumapili haitakuwa na mashabiki kutumikia adhabu ya CAF. Kilichosababisha ni mchezo ni dhidi ya Al Masry, kuna shabiki aliingia uwanjani na kuna mashabiki waliwasha moto. Adhabu hiyo inakwenda pamoja na faini ya Dola 50,000 kama Tsh. 120 milioni hivi.

“Niwaase mashabiki wenzangu wa Simba, uache vitendo vya vurugu uwanjani. Kwanza tuanze ulinzi wa wenyewe kwa wenyewe ukiona mtu anataka kuwasha zile fire works mzuie, ukiona mtu anataka kuingia uwanjani tushirikiane kumzuia ikiwezekana kumtoa uwanjani. Angalia mechi kama hii tunakwenda uwanjani bila mashabiki. Hatupo hapa kulaumiana ila kukumbushana,”.