Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso, amewasili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, kama Mgeni Rasmi katika kilele cha Wiki ya Simba (Simba Day 2025).
Katika tukio hilo kubwa linaloendelea hivi sasa, Waziri Aweso ameungana na viongozi wa Simba SC pamoja na maelfu ya mashabiki waliomiminika kushuhudia burudani, utambulisho wa kikosi kipya cha msimu huu na shamrashamra zinazotambulisha heshima na hadhi ya klabu hiyo.
Simba Day, ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka, ni sehemu ya utamaduni wa klabu hiyo kongwe barani Afrika, ikileta pamoja wapenzi wa soka na burudani huku ikitoa taswira ya mshikamano mkubwa kati ya klabu na mashabiki wake.
Kilele cha maadhimisho ya mwaka huu kimeambatana na burudani kutoka kwa wasanii wakubwa, pamoja na matarajio makubwa ya mashabiki kuhusu kikosi kipya cha Simba kitakachoingia dimbani kwenye michuano ya ndani na kimataifa msimu wa 2025/26.