SIMBA SC YAZINDUA JEZI, MSEMAJI WA SERIKALI AWAOMBA KUNUNUA ORIGINAL

SIMBA SC imezindua rasmi uzi wake mpya kuelekea msimu wa 2025/26 Agosti 31 2025 katika ukumbi wa Super Dome, Masaki na mgeni rasmi alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Gerson Msigwa.

Msigwa amesema kuwa ni muhimu kwa mashabiki wa Simba SC kuhakikisha kuwa wanapata bidhaa original na sio feki kutokana na gharama kubwa ambazo zipo katika kuendesha timu na ubunifu ambao umetumika kwenye kutengeneza uzi mpya.

Amebainisha kuwa anatambua gharama zilivyo katika kuhakikisha mipango inakwenda sawa ndani ya timu kwa kuwa hata yeye aliwahi kuwa kiongozi wa Majimaji ya Songea.

“Jezi ni nzuri na pongezi kwa kazi ambayo imefanywa na JayRutty na Diadora. Kazi kubwa na jezi nimeona ni nzuri hakika wanapaswa pongezi na hasa kwenye eneo la kubainisha jezi feki na ambayo haitakuwa feki hii ni hatua kubwa .

“Ni muhimu mashabiki kununua jezi halisi ya Simba SC na sio zinazotengenezwa na wahuni, inawezekana na itakuwa ni faida kwa Simba SC ili ijiendeshe kwa faida. Kuna gharama kubwa kwenye kuendesha timu na mimi nilishawaji kuwa kiongozi wa Majimaji, hakika kuna wakati mambo yalikuwa magumu tulikuwa tunarudi nyumbani kuchukua sembe ili wachezaji wapate chakula,”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jayrutty Investment, Joseph Rwegasira amesema kuwa kazi kubwa imefanyika katika uzi mpya na ubora wake ni mkubwa kutokana na uwekezaji ambao umefanyika.

“Ukitazama jezi mpya ni bora kutokana na malighafi ambazo zimetumika, kila nembo ambayo ipo imewekwa katika umakini mkubwa na tulikuwa tunafanyia kazi kila wazo ambalo tunapata kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata kazi nzuri.

“Kuna code ambayo ipo kwenye jezi hii inakufanya utambue kwamba jezi ni feki ama original hivyo ni muhimu kuzingatia hilo na kwa sasa kila sehemu jezi zipo na tunasambaza kwa njia ya Posta jambo ambalo linafanya iwe rahisi kuwafikia Watanzania wote.”

Katika uzinduzi huo, kulikuwa na burudani mbalimbali ikiwa ni muziki wa band live, msanii Ali Kiba alikuwa ni zawadi kwa wageni kwa kuwa hakuna ambaye alitarajia uwepo wake na alitumbuiza nyimbo pendwa ikiwa ni ile ya Unyama ni Mwingi.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo na Moyo Wangu Unavuja Damu.  Kuvipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371.

Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Msichana wa Maisha Yangu, jiandae kuipata.