WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye anga la kimataifa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba SC bado hawajamaliza usajili licha ya Agosti 21 kumtambulisha nyota mpya.
Timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids kambi yake kwa maandalizi ya msimu mpya wa 2025/26 ipo nchini Misri na wanatarajia kurejea muda sio mrefu katika ardhi ya Tanzania.
Neo Maema raia wa Afrika Kusini alitambulishwa usiku wa Agosti 21 2025 huyu ni kiungo mshambuliaji ambaye alikuwa anacheza Mamelod Sundowns.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC amesema kuwa bado utambulisho wa wachezaji wapya unaendelea kwa ajili ya msimu ujao.
“Simba bado kuna wachezaji hatujawatambulisha na hao waliobaki tukitambulisha mmoja tu kila mwenye simu ya ‘Smartphone’, basi ‘Protector’ itapasuka bila kuidondosha ni wachezaji kweli.
“Huyu mmoja ni mjukuu wa Madiba kutoka Sauzi lakini katika faili langu kuna mchezaji mmoja yupo vizuri kwelikweli. Wanasimba tuzidi kuwa pamoja.”