UONGOZI wa Simba SC umetaja siku rasmi itakayokuwa ni maalumu kwa uzinduzi wa uzi mpya wa timu hiyo kuelekea msimu mpya wa 2025/26 unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC ameweka wazi kuwa uzinduzi wa uzi mpya utakuwa watofauti kidogo kutokana na mpango kazi uliopo.
“Jezi za Simba msimu huu tutazindua kwa namna tofauti kidogo, ipo namna ambayo tumezoea jezi huwa zinazinduliwa lakini safari hii sababu tuna mdhamini mpya wa jezi kampuni ya JayRutty akishirikiana na kampuni ya kimataifa ya Diadora tukaamua kufanya kitu kipya chenye mvuto kwa jamii na biashara ya jezi kuwa na mvuto wa tofauti.
“Jezi za Simba SC msimu wa 2025/26 zitazinduliwa tarehe 27/Agosti/2025, jezi zitazinduliwa majira ya saa 1:00 usiku na shughuli itafanyika kwenye ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki. Safari hii tumefanya kuwa tukio kubwa, tukio lenye hadhi ya ushua na kulifanya kuwa tukio bora ambalo litakutanisha wadau wakubwa wa Simba Sports Club na ambao wanataka kununua jezi ya Simba SC baada ya kuzinduliwa.
“Siku hiyo wenye dhamira ya kushuhudia uzinduzi wa jezi na baada ya uzinduzi hapo hapo ukumbini watapewa jezi zao tatu. Kwanza kutakuwa na wasanii mbalimbali, tutakuja kuwatangazia msanii mmoja baada ya mwingine lakini pia kutakuwa na live band, kutakuwa na vinywaji pamoja na vyakula vya kutosha. Kwa upekee na kulifanya kuwa bora kabisa kutakuwa na mgeni rasmi ambaye ni mchezaji wa zamani bora barani Afrika, ambaye ametikisa Afrika, ambaye amefanya makubwa kwenye mpira, mchezaji ambaye anajulikana dunia nzima ndiye atakuwa mgeni rasmi na ndio ataitambulisha jezi kwa mara ya kwanza.
“Yeyote ambaye atahitaji kuhudhuria tukio hili la uzinduzi wa jezi na kuwa mtu wa kwanza kuona jezi ya Simba SC msimu huu atalipa Tsh. 250,000. Akishalipa hiyo fedha yote ambayo atapata ndani ya ukumbi ni juu yetu na baada ya hapo atapewa jezi zote tatu za msimu huu. Vyote hivyo atakabidhiwa hapo hapo ukumbini.
“Mara baada ya uzinduzi huo, jezi za Simba SC zitaanza kuuzwa kwenye maduka yote ambayo yameshaweka pre order na wanasubiri mzigo wao. Wakati zoezi la uzinduzi linafanyika Super Dome, kwenye maduka muda huo huo watakuwa wanachukua mizigo yao kwenda kuwauzia Wanasimba. JayRutyy ameleta jezi nyingi kwelikweli, uwe Simba SC, usiwe Simba SC zinamtosha kila Mtanzania,” amesema Ahmed Ally.