Hong Kong – Klabu ya Arsenal imejikuta ikianza maandalizi ya msimu mpya kwa kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa wapinzani wao wa jadi, Tottenham Hotspur, katika mchezo wa kirafiki uliopigwa usiku wa kuamkia leo jijini Hong Kong.
Pape Matar Sarr, kiungo mahiri kutoka Senegal, ndiye aliyeibeba Spurs baada ya kufunga bao pekee la mchezo kwa shuti kali la mbali kipindi cha kwanza, akimshinda mlinda mlango wa Arsenal na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Tottenham waliokuwepo uwanjani.
Licha ya juhudi za Arsenal kusaka bao la kusawazisha katika kipindi cha pili, walijikuta wakipambana na ukuta imara wa Spurs uliosimama imara hadi dakika ya mwisho. Viktor Gyökeres, aliyesajiliwa hivi karibuni, aliingia dakika za lala salama lakini hakubadilisha matokeo.