Klabu ya Arsenal imetangaza rasmi kumsajili beki kinda mwenye kipaji, Cristhian Mosquera, kutoka klabu ya Valencia ya Hispania kwa ada ya uhamisho inayokadiriwa kufikia Euro milioni 15 .
Mosquera, mwenye umri wa miaka 21, amesaini mkataba wa miaka mitano na chaguo la kuongezewa mwaka mmoja zaidi, ikiwa ni ishara kuwa kocha Mikel Arteta ana mpango wa muda mrefu naye kwenye kikosi cha The Gunners.
Beki huyo wa kulia ambaye pia ana uwezo wa kucheza nafasi zote kwenye safu ya ulinzi, anajulikana kwa spidi, nguvu ya mwili, na utulivu mkubwa akiwa na mpira, sifa ambazo zimevutia Arsenal kumchukua mapema kabla ya klabu nyingine kubwa kumuwahi.
Mosquera pia ni sehemu ya kikosi cha vijana cha timu ya taifa ya Uhispania chini ya miaka 21, ambapo ameonyesha kiwango kikubwa, na kutajwa kuwa mmoja wa mabeki wa baadaye wa kuaminiwa na timu ya wakubwa ya La Roja.
Mashabiki wa Arsenal tayari wameanza kuonyesha furaha yao kupitia mitandao ya kijamii, wakiamini kuwa Mosquera ataleta ushindani na nguvu mpya kwenye safu ya ulinzi, hasa kwa kuzingatia majukumu makubwa yanayowakabili kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu ya England na mashindano ya Ulaya.