YANGA YAMNASA CASEMIRO WA ZANZIBAR KUTOKA MLANDEGE!

Klabu ya Yanga imeendelea kujiimarisha kuelekea msimu mpya baada ya kumtambulisha rasmi kiungo mkabaji wa Mlandege, Abdulnassir Mohammed Abdallah, maarufu kama “Casemiro”, kwa mkataba wa miaka mitatu.

Usajili wa kiungo huyo mahiri ulimalizika tangu Julai 2, 2025, lakini klabu hiyo imemtambulisha rasmi leo, ikiwa ni sehemu ya mipango yao ya kusuka kikosi imara na chenye ushindani wa hali ya juu.

Katika kumsajili, Yanga walishinda vita kali ya saini yake dhidi ya klabu kama Azam FC, JKT Tanzania na Singida Black Stars, ambazo zote zilikuwa kwenye harakati za kumchukua kiungo huyo tegemeo kutoka Zanzibar.

Abdulnassir, anayefahamika kwa jina la utani la “Casemiro” kutokana na aina yake ya uchezaji wa kukaba kwa ufanisi, ni kipaji kipya kilichotoka visiwani Zanzibar, na anaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuziba nafasi ya kiungo mkabaji ndani ya kikosi cha Wananchi.

Usajili huu unaashiria dhamira ya Yanga ya kuendelea kuwa na safu thabiti ya kiungo, huku wakijihakikishia nguvu mpya itakayowasaidia katika mashindano ya ndani na ya kimataifa.