KAPOMBE AMWAGA WINO SIMBA, AJIPANGA KWA MSIMU MPYA

Shomari Kapombe anaripotiwa kuwa tayari amekubaliana na klabu ya Simba kuhusu kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuwatumikia Wekundu wa Msimbazi, licha ya mkataba wake wa awali kumalizika rasmi Juni 30, 2025.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya klabu vinadai kuwa hakuna presha yoyote baina ya pande hizo mbili, na kwamba mkataba mpya upo tayari na utatiwa saini muda wowote kuanzia sasa.

Kapombe, ambaye kwa sasa yupo kwenye mipango ya moja kwa moja ya kocha mkuu Fadlu Davids, anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji ambao kocha huyo anawategemea mno katika kikosi chake. Inadaiwa kuwa Davids alisisitiza asiondoke, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa maamuzi ya Kapombe kubaki klabuni.

Kitetesi kingine kinachozidi kushika kasi ni kwamba beki huyo mwenye umri wa miaka 33 ana nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa nahodha mpya wa klabu kuelekea msimu ujao, akichukua mikoba ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.