BARCELONA YAKARIBIA KUKAMILISHA USAJILI WA RASHFORD KWA MKOPO

Klabu ya FC Barcelona imefikia makubaliano ya awali na Manchester United kwa ajili ya kumsajili Marcus Rashford kwa mkataba wa mkopo, ikiwa ni hatua kubwa kuelekea usajili wa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England kuelekea La Liga.

Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na klabu hizo, mazungumzo ya awali yamekuwa mazuri na ya kuleta matumaini, huku hatua inayofuata ikiwa ni kukamilisha maelewano kuhusu asilimia ya mshahara wa Rashford ambayo Barcelona itabeba katika kipindi cha mkopo.

Aidha, klabu hizo mbili bado zipo kwenye mazungumzo kuhusu kipengele cha fidia, iwapo Barcelona haitatumia chaguo la kumnunua moja kwa moja mchezaji huyo mara baada ya mkopo wake kumalizika.

Marcus Rashford, ambaye amekua chini ya kiwango msimu uliopita katika Ligi Kuu ya England, anaonekana kutafuta changamoto mpya huku Barcelona wakiona nafasi ya kumuamsha upya kwenye mfumo wao wa ushambuliaji.

Iwapo dili hili litakamilika, Rashford ataungana na mastaa wengine chipukizi wa Barca na huenda akawa sehemu muhimu ya kikosi cha kocha Hansi Flick kwa msimu wa 2025/26.