MAVAMBO AMALIZA SAFARI YAKE SIMBA SC, ATOA UJUMBE WA KUAGA

Kiungo fundi wa kimataifa, Debora Fernandes Mavambo (24), mwenye uraia pacha wa Congo-Brazzaville na Gabon, ameaga rasmi klabu ya Simba SC, takribani mwaka mmoja tu tangu asajiliwe kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Mutondo Stars ya Zambia.

Mavambo ambaye anachezea timu ya taifa ya Gabon, ametangaza kuondoka kwake kupitia ujumbe wa kuushukuru uongozi na mashabiki wa klabu hiyo maarufu ya Msimbazi, akisisitiza kuwa ataikumbuka Simba daima kwa sapoti na mapokezi aliyoyapata wakati wote wa uwepo wake.

“Asante sana familia ya Simba SC kwa sapoti yao katika kipindi chote nilichokuwa ndani ya klabu hii. Hakika nitaikumbuka klabu hii, mashabiki na viongozi wote wa Simba Sport Club,” alisema Mavambo kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii.

Nyota huyo mwenye kipaji kikubwa katika eneo la kiungo cha kati, alisajiliwa na Simba kwa matarajio makubwa ya kuimarisha safu ya kiungo lakini safari yake imekatika kabla ya kukamilika kwa mkataba wake wa awali.

Hadi sasa haijafahamika rasmi sababu za kuondoka kwake mapema, lakini taarifa za ndani ya klabu zinaashiria uwezekano wa pande hizo mbili kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba kwa makubaliano maalum.

Kuondoka kwa Mavambo kunafungua nafasi katika kikosi cha Simba kinachoendelea na mchakato wa usajili na maandalizi ya msimu mpya wa 2025/26, ambapo klabu hiyo imekuwa ikifanya mabadiliko kadhaa ndani ya kikosi chake kuelekea kampeni mpya za ndani na kimataifa.