Kinda mahiri wa FC Barcelona, Lamine Yamal, ametia saini mkataba mpya wa muda mrefu na klabu hiyo, ambao utamuweka Camp Nou hadi tarehe 30 Juni 2031. Tangazo hilo lilifanywa rasmi na Barcelona leo Jumanne, na limeambatana na hatua ya kihistoria ambapo Yamal amekabidhiwa rasmi jezi namba 10, namba yenye heshima kubwa katika historia ya klabu hiyo.
Jezi hiyo imewahi kuvaliwa na vigogo wa soka kama Ronaldinho Gaucho, Lionel Messi, na hivi karibuni Ansu Fati, na sasa ni zamu ya Yamal kuibeba, ishara ya imani kubwa ya klabu kwake.
Yamal, ambaye hivi karibuni alitimiza miaka 18, amekuwa gumzo barani Ulaya kutokana na uwezo wake wa kipekee uwanjani. Amevunja rekodi mbalimbali akiwa na umri mdogo katika La Liga, na ameng’ara pia katika mashindano ya kimataifa ikiwemo UEFA Euro 2024, ambapo alionyesha kiwango cha juu licha ya umri wake mdogo.
Katika hafla ya kusaini mkataba huo, iliyofanyika kwenye ofisi za klabu ya Barcelona, Yamal alisindikizwa na bibi yake mpendwa, huku tukio hilo likihudhuriwa pia na Rais wa klabu Joan Laporta pamoja na Mkurugenzi wa Michezo Deco.
Mara baada ya kusaini mkataba huo, Yamal alizungumza kwa hisia kali akisema:
“Barça ni klabu ya maisha yangu. Ndoto yangu imetimia. Nafurahi sana kuona familia yangu hapa leo. Nitapambana kwa ajili ya klabu hii ambayo imenilea.”