Dar es Salaam, Julai 10, 2025 – Kesi namba 8323/2025 inayohusu mgawanyo wa rasilimali za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imeahirishwa rasmi na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, hadi Jumatatu, Julai 14 saa nne asubuhi.
Shauri hilo limesitishwa kufuatia maombi ya mawakili wa upande wa waleta maombi waliotaka muda wa kupitia barua ya upande wa wajibu maombi, ambayo iliwasilishwa mahakamani mapema leo.
Barua hiyo, iliyowasilishwa na Wakili Mpale Mpoki kwa niaba ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, ilimwomba Naibu Msajili wa Mahakama kuhakikisha kuwa Jaji Hamidu Mwanga ajiondoe kusikiliza kesi hiyo kwa sababu ambazo hazikuelezwa kwa kina mahakamani hapo.
Akizungumza mbele ya mahakama, Wakili Mpoki alieleza kuwa walichelewa kuwasilisha nakala kwa upande wa waleta maombi kwa kuwa walidhani barua hiyo ilikuwa ya matumizi ya mahakama pekee. Hata hivyo, upande wa waleta maombi uliomba muda wa kutosha kuisoma na kuitafakari barua hiyo kabla ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo.
Kucheleweshwa kwa kesi hiyo kunasababisha pia kusitishwa kwa usikilizwaji wa maombi madogo yaliyowasilishwa na upande wa CHADEMA, wakitaka mahakama ifute uamuzi wa awali wa Jaji Mwanga wa Juni 10, uliosimamisha shughuli za chama hicho.
Jaji Hamidu Mwanga ameieleza mahakama kuwa maombi hayo madogo hayawezi kushughulikiwa hadi pale itakapotolewa uamuzi rasmi kama ataendelea na usikilizaji wa kesi au la.
Kesi hiyo inaendelea kufuatiliwa kwa karibu na wadau wa kisiasa, wanachama wa CHADEMA na wachambuzi wa sheria, kutokana na uzito wake katika mustakabali wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.