RUBEN NEVES ASAFIRI KUTOKA MAREKANI HADI URENO KWA MAZISHI YA JOTA NA SILVA

Ruben Neves Aungana na Waombolezaji Ureno Kuwapa Heshima za Mwisho Diogo Jota na André Silva

Kiungo nyota wa kimataifa, Ruben Neves, ambaye usiku wa kuamkia leo alikuwa nchini Marekani akicheza mechi, amewasili kwa haraka nchini Ureno kushiriki mazishi ya wachezaji wenzake, Diogo Jota na André Silva, waliotangulia mbele ya haki.

Nahodha huyo wa zamani wa Wolves ameungana na wachezaji wenzake wa zamani na wa sasa, familia pamoja na mashabiki katika kutoa heshima za mwisho kwa mastaa hao waliowahi kuwa sehemu muhimu ya timu ya taifa ya Ureno na klabu walizozitumikia.

Katika ibada hiyo ya maombolezo, Neves alionekana akiwa miongoni mwa waliobeba jeneza kuingia kanisani – tukio lililowaacha wengi wakiwa na huzuni kubwa. Hisia zilitawala ibada hiyo, huku nyuso za huzuni na machozi zikithibitisha namna maisha ya Jota na Silva yalivyogusa mioyo ya mashabiki na wapenzi wa soka duniani.

Kifo cha wachezaji hao wawili kimetikisa ulimwengu wa soka, na tukio hili limekuwa ishara ya mshikamano, upendo na heshima miongoni mwa familia ya mpira wa miguu.