KATIKA kurejesha kwa jamii wachezaji, Nassor Kapama ambaye ni kiungo wa Kagera Sugar pamoja na mshambuliaji wa JKT Tanzania, Mohammed Bakari ‘Muddy Beka’ Julai 12, mwaka huu wanatarajia kucheza mechi ya hisani ikiwa na lengo maalum la kusaidia watu wasiojiweza.
Mechi hiyo imeeandaliwa maalum na nyota hao ambao wanashiriki Ligi Kuu Bara ambapo itafanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kigamboni, Dar huku kiasi chote ambacho kitapatikana katika mechi hiyo kitatolewa kwa wahitaji.
Muandaaji wa mchezo huo, Kapama amesema, kuwa maandalizi ya mchezo huo hadi sasa yanaendelea ambapo lengo kubwa la kufanya hivyo ni kutaka kusaidia wanajamii wa eneo hilo.
“Hadi sasa kila kitu kinaendelea vizuri kuhusiana na mchezo huu ambao lengo kubwa ni kurudisha kwa jamii ambayo tunakaa nayo lakini pia kutoa kile kidogo ambacho tunacho.
“Fedha ambazo zitapatikana katika mchezo huu basi zitaenda kwa kundi hilo ambapo tunakaribisha watu na kampuni kuja kudhamini mchezo wetu huu ambao tunatarajia kutakuwa na mastaa mbalimbali wa ligi kuu.
“Kwenye mechi yetu hii kutakuwa na timu ya Kapama na Timu ya Muddy Beka na baadhi ya mastaa ambao watakuwa sehemu ya mchezo huu ni Mkude (Jonas), Erasto Nyoni, Hassan Dilunga, Joash Onyango, Abdultwalib Mshery, Hussein Kazi, Abal Kassim na wengine zaidi tutawatambulisha kwa kila siku zinavyokwenda,” alisema Kapama.