Simba SC imevuna pointi tatu kwenye mchezo wa ligi mzunguko wa pili dhidi ya Singida Black Stars, Mei 28 2025, Uwanja wa KMC Complex.
Baada ya dakika 90 ubao umesoma Simba SC 1-0 Singida Black Stars ikiwa ni mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa kwa wababe hawa wawili.
Bao pekee la ushindi limepachikwa na Steven Mukwala dakika ya 42 akitumia pasi ya kiungo mshambuliaji Jean Ahoua ambalo limedumu mpaka mwisho wa mchezo.
Singida Black Stars walikuwa wakifanya mashambulizi yao kupitia kwa Jonathan Sowah ambaye ni kinara wakucheka na nyavu ndani ya Singida Black Stars akiwa na mabao 11.
Bahati haikuwa upande wake kwa kuwa majaribio yake mawili yaliokolewa na kipa Moussa Camara ambaye alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi Elly Sasii dakika ya 82 kwa kile alichotafsri kuwa alikuwa anapoteza muda.
Sowah naye alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 90 baada ya kuonekana amemchezea faulo kipa Camara ambaye alikuwa anaokoa hatari iliyokuwa inakwenda katika lango la Simba SC.
Simba SC inafikisha pointi 72 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo vinara ni Yanga SC wenye pointi 73 wote wakiwa wamecheza jumla ya mechi 27.
Wababe hawa wanatarajiwa kukutana Juni 15 2025 kwenye Kariakoo Dabi ikiwa ni mzunguko wa pili msimu wa 2024/25.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu itazinduliwa rasmi Julai 24 2025 usipange kukosa.