SIMBA HAWAJAKATA TAMAA KIMATAIFA, KAZI INAENDELEA

SHOMARI Kapombe, nahodha msaidizi wa Simba SC na beki wa kikosi hicho ameweka wazi kuwa wanatambua wamepoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane lakini watapambana kupata matokeo mchezo wa pili.

Ikumbukwe kwamba Mei 17 2025 kwenye mchezo wa hatua ya fainali ya kwanza uliochezwa nchini Morocco baada ya dakika 90 ubao ulisoma RS Berkane 2-0 Simba SC, mchezo wa pili utaamua nani atatwaa taji hilo ambapo tayari RS Berkane wametanguliza mguu mmoja kwenye hatua ya kutwaa taji hilo.

Kapombe alianza kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa ugenini na alifanya kazi kubwa katika kutimiza majukumu yake eneo la ulinzi ambalo lilikuwa kwenye wakati mgumu kutokana na safu ya ushambuliaji ya RS Berkane kuwa na kasi mwanzo mwisho.

“Tunatambua kwamba hatujapata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu dhidi ya RS Berkane tukiwa ugenini, kazi bado haijaisha hivyo matokeo ambayo yametokea ugenini tunasahau na tunaanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu ujao wa fainali tukiwa nyumbani.”

Simba ili itwae taji la Kombe la Shirikisho Afrika kwenye mchezo wa nyumbani unaotarajiwa kuchezwa Mei 25 lazima wapate ushindi wa mabao 3 na wapambane safu ya ulinzi isiruhusu bao.

Kauli mbiu ya Simba SC kwenye mechi za kimataifa inakwenda na msemo unaosema Hii Tunabeba. Tayari kikosi cha Simba SC kimerejea Dar kwa maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa fainali.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu itazinduliwa rasmi Julai 24 2025 usipange kukosa.