YANGA MABINGWA WA KOMBE LA MUUNGANO

ZANZIBAR-Young Africans Sports Club (Yanga SC) ya jijini Dar es Salaam imetwaa taji la saba la Michuano ya Kombe la Muungano.

Ni baada ya Mei 1, 2025 katika dimba la Gombani lililopo Kisiwani Pemba kuwachapa Maafande wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) kwa bao 1-0. Bao pekee la Maxi Mpia Nzengeli lilipatikana dakika ya 46′.

Yanga ilitinga fainali ya michuano hiyo baada ya kuwatoa Zimamoto FC kwa mikwaju ya penalti 3-1, baada ya dakika 90 za nusu fainali yao kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Aidha,JKU walifuzu fainali baada ya kuwatupa nje Azam FC ya jijini Dar es Salaam kwa mabao 2-1.

Muungano Cup ni mahususi katika kuadhimisha miaka ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano huo ambao ni zao la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka huu wa 2025 umefikisha miaka 61.

Ikumbukwe Yanga SC iliwahi kutwaa Kombe la Muungano mwaka 1983, 1987, 1991, 1996, 1997 na 2000.

Kombe hili ambalo lilianza rasmi mwaka 1982 lengo ni kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kutoa usawa wa kiuwakilishi katika michuano ya kimataifa ya vilabu.

Ni kutokana na Tanzania Bara kuwa na ligi yake na Zanzibar kuwa na ligi yake huku upande wa visiwani ukiwa sio mwanachama wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).