Klabu ya Al Ahly ya Misri imetangaza kuachana na kocha Marcel Koller baada ya kutolewa katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 64 alipata lawama kubwa baada ya mabingwa watetezi kutolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa kanuni ya bao la ugenini, baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mechi ya marudiano jijini Cairo Ijumaa, kufuatia sare tasa jijini Pretoria.
Chupa za maji zilirushwa kutoka majukwaani zikielekezwa kwa raia huyo wa Uswisi alipoondoka uwanjani baada ya filimbi ya mwisho.
“Kutokana na hali ya dharura na kwa kuzingatia uhusiano wa kipekee uliodhihirika katika nafasi nyingi za awali, klabu kwa sasa inazungumza na kocha huyo kuhusu kusitisha mkataba kwa makubaliano ya pande zote kwa njia inayoheshimu klabu na kocha wake,” klabu ilisema katika taarifa.
Tangu achukue nafasi hiyo mwaka 2022, kocha huyo wa zamani wa FC Basel na FC Koln aliiongoza Al Ahly kutwaa mataji kadhaa, ikiwemo mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa.