MABINGWA watetezi wa CRDB Federation Cup, Yanga chini ya Kocha Mkuu, Miloud Hamdi watakuwa na kibarua cha kusaka ushindi dhidi ya Stand United, Uwanja wa KMC Complex.
Yanga metoka kupata ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika dhidi ya Azam FC kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amebainisha kuwa wanahitaji kufanya vizuri kwenye mechi zote ambazo watacheza ili kufikia malengo ambayo wanayo kutwaa mataji yao waliyochukua msimu uliopita wa 2023/24.
“Wapinzani wetu tunawaheshimu na tunatambua ni timu ambayo inahitaji matokeo mazuri, tumetoka kupata ushindi kwenye mchezo wetu uliopita dhidi ya Azam FC hivyo ile morali ya ushindi bado ipo kwa wachezaji na benchi la ufundi.
“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kwenye mchezo wetu kwa kuwa kikubwa ambacho tunahitaji kuona wakipata furaha wakiwa uwanjani.”
Viingilio kwenye mchezo wa leo ni 10,000 mzunguko na VIP ni 20,000 mchezo unatarajiwa kuanza saa 10:00 jioni.